Ukimtizama kwa makini mshambuliaji wa Yanga Michael Sarpong, utabaini ni mchezaji anayeonekana kuwa na uwezo mzuri tu ndani ya dimba lakini kwa sasa anapita katika nyakati mbaya
Uongozi wa Yanga pamoja na wadhamini GSM walifanya jambo la maana kuendelea kumbakisha Sarpong kikosini licha ya presha ya mashabiki waliotamani kumuona nyota huyo anaachwa kwenye dirisha dogo
Sarpong amefunga mabao manne msimu huu katika ligi kuu, sio wastani mbaya wa mabao ukilinganisha na aneyeongoza John Bocco mwenye mabao nane
Wengi hawakufurahishwa na kiwango alichoonyesha kwenye michuano ya kombe la Mapinduzi, lakini naamini ni nyakati mbaya tu kwake ambazo kila mchezaji huwa anapitia
Wanayanga hawapaswi kuwa na shaka na mwamba huyu, ana takwimu nzuri tu za kufunga mabao katika ligi alizocheza nchi nyingine
Timu ya mwisho kuitumikia kabla ya kusajiliwa na Yanga ni Rayon Sports, ambako alifunga mabao 24 katika misimu miwili
Msimu wake wa kwanza alifunga mabao 16 na msimu wake wa pili akafunga mabao nane, msimu ambao hakumaliza mkataba baada ya timu hiyo kuvunja mkataba wake kutokana na mvutano uliojitokeza baina yake na uongozi
Aidha ujio wa mshambuliaji Fiston Abdul Razak unaweza ukamuongezea changamoto kwani atakabiliwa na ushindani wa kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza
Wakati huu ambao ligi imesimama ni nafasi kwake kunoa makali ili arudi upya mwezi ujao ligi itakaporejea