Simba walizua Al Ahly, waarabu waanza kuzozana

 

KASI ya Simba kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika bado ni tatizo kwa Al Ahly ya Misri chini ya Kocha Msauzi, Pitso Motsimane.

Kitendo cha Bingwa huyo mtetezi wa Afrika kushindwa kuongoza kundi lake mpaka sasa pamoja na kutokuwa na uhakika wa moja kwa moja wa kufuzu robofainali kumewashtua mastaa wengi wa zamani wa klabu hiyo maarufu.

Maveterani wa Ahly bado wanaamini kwamba kipigo cha bao 1-0 ilichopata Ahly mbele ya Simba Jijini Dar es Salaam ni makosa ya kiufundi ya Pitso.

Lakini wakaenda mbali zaidi kwa kusisitiza kwamba wachezaji wa timu hiyo wanacheza chini ya kiwango kwa sasa na hawamsaidii Pitso. Simba inaongoza Kundi A la Ligi ya Mabingwa Afrika kwa pointi 10, Ahly pointi saba, AS Vita nne na Al Merrikh pointi moja.

Staa wa zamani wa Ahly, Wael Gomaa amedai kwamba wachezaji hawajitumi katika siku za hivikaribuni kuanzia kimataifa mpaka kwenye ligi ya ndani. Amedai kwamba kipigo dhidi ya Simba kilikuwa muafaka ili kuonyesha udhaifu ndani ya timu pamoja na upangaji wa kikosi na mabadiliko yenye kasoro ambayo hufanywa na Pitso mara kadhaa.

“Alhly ina wachezaji bora duniani haipaswi kufanya vibaya, angalia hata mabadiliko yanayofanywa na Pitso wakati mwingine yanapunguza kasi ya ushindani, sikatai ni Kocha mzuri lakini bado kuna changamoto kubwa,”alisema beki huyo wa zamani wa Ahly.

Mbali na staa huyo, wachezaji kadhaa wa zamani wa Alhy wamekuwa wakikosoa staili ya uchezaji na ubora wa kikosi hicho tangu kuwasili kwa Pitso. Wachambuzi mbalimbali wamekuwa wakimkosoa kwa madai kwamba amekosa kikosi cha kwanza tangu ajiunge na kikosi hicho.

Beki wa zamani wa Afrika Kusini,Mark Fish anaamini pamoja na changamoto Pitso alizonazo kwenye kundi lake msimu huu bado ana nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwavile ni muda mfupi tangu achukue nafasi hiyo nyeti.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Contact Form